//
you're reading...
Uncategorized

WHY SAY NO TO DRAFT CONSTITUTION IN KENYA

BY KOIGI WAMWERE OF CHAMA CHA MWANANCHI

Dhamiri Ya Sauti Ya Mwananchi Inasema La Kwa Katiba Mpya Isiyosawazisha Watu, Tabaka, Wala Dini

Ijapokuwa Dhamiri inaunga mkono dhana ya katiba mpya, hailii, bora katiba mpya. Inalilia katiba mpya bora.

Ili tupate katiba mpya bora, nchi hii ilihitaji na bado inahitaji mjadala wa kitaifa utakaochangiwa na kila mwenye maoni kuhusu katiba mpya bila kubaguliwa au kupendelewa na vyombo vya habari ambavyo kwa sasa vimekataa kuruhusu mjadala wa wote kuhusu katiba mpya.

Ili kupata katiba mpya bora, Dhamiri pia haina tashwishi kwamba Wakenya lazima watazame sio tu yaliyomo katika katiba mpya lakini pia yale ambayo hayamo. Dhamiri inasema hili kwa sababu inahisi, yaliyoachwa nje ya katiba mpya ni muhimu kuliko yaliyomo.

Ili tuelewe katiba mpya, lazima tujiulize, ni nani walioiandika na waliiandikia nani?

Kwa jumla, Dhamiri inaamini, ingawa kwa kutojua, maskini wataipigia kura, katiba mpya ni katiba ya matajiri sio ya mafukara ambao ndio wengi nchini na wanaostahili kuimiliki kwa mujibu wa utawala wa walio wengi.

Ya kwamba katiba mpya haisheheni maslahi ya maskini linaonyeshwa vizuri na kibonzo au katuni ya gazeti la Nation, kinachoonyesha Yesu-Wanjiku ambaye ni maskini akibebeshwa msalaba wa katiba mpya huku akihimizwa aongeze kasi ya kwenda Golgotha au machinjioni yake na wabunge wanaobeba rungu, viongozi wa dini waliovalia misalaba, matajiri wenye nyuso za mbweha, wasomi na wafanyabiashara wanaobeba mapanga, mishale na bunduki zinazopiga risasi juu. Ajabu ni kwamba Wanjiku uyu huyu anaebeba msalaba wa katiba mpya ndiye atakayeipigia kura ianze kumnyanyasa na kumnyonya ili marais, mawaziri, magavana na wabunge walioongezeka mara kadha katika bunge la taifa, seneti na mabunge ya county wapate mishahara yao ya juu. Kwa bahati mbaya, unaweza kumpeleka ng’ombe mtoni, lakini huwezi kumlazimisha anyue maji. Dhamiri nayo inaweza kumtanadharisha Wanjiku juu ya hatari za katiba mpya, lakini haiwezi kumlazimisha aikatae.

Kama katika nchi ya Israeli iliyoandikiwa katiba ya Amri Kumi za Mungu na Mungu mwenyewe huku akishirikisha Musa peke yake, kwa sababu ya utakatifu wake, katika Kenya, badala ya kuandikiwa katiba mpya na waliotakasika zaidi miongoni mwetu, tuliwapa walio wachafu zaidi watwandikie katiba mpya.

Ya kwamba tunaandikiwa katiba na wabunge mafisadi, wakabila, madikteta na washukiwa wanaochunguzwa na Moreno Ocampo kwa kupanga na kufadhili vita na mauaji ya kimbari au genocide, kunaonyesha hatuithamini sana katiba mpya kama tunavyodai. Katika nchi zingine, watu walioandikia Kenya katiba mpya hawangeruhusiwa wakaribie au waiguse rasimu yake kwa hofu yakuitia najisi.

Kuongeza chumvi kwenye kidonda, mafisadi wanaoandika katiba mpya ndio ao hao watakaojilipa mabilioni ya pesa za serikali ili mashirika yao, magazeti, radio na runinga zao zituletee elimu yakutukubalisha katiba hio. Nani hajui anayemlipa mpiga nzumari ndiye huchagua wimbo? Mradi katiba mpya iko mikononi ya mafisadi, yenyewe na elimu kuihusu, zote zitakuwa fisadi na potofu.

Kweli Wakenya wanawezaje kutarajia katiba ya kuwaokoa kama inaandikwa na viongozi na wasomi fisadi, wale wale wanaowafisha na kuwazika mchana kweupe? Kama mti fisadi huzaa matunda fisadi, viongozi na wasomi fisadi nao wamezaa katiba fisadi.

Kwa sababu watu walioandika katiba mpya, kiitikadi ni maadui wa maskini, kamwe katiba yao haibebi sura zinazoshughulikia matatizo ya umaskini, ukabila, ufisadi na ubepari unaotuzalia matatizo yetu yote. Kwa sababu ya kushughulikia tu ugavi wa mamlaka na rasilmali kati ya viongozi wa makabila tofauti, matajiri na wasomi, kabisa katiba hii haitoshi kuitwa katiba ya watu wote. Ni katiba ya viongozi wa makabila, matajiri na wasomi.

Ingawa wengine wanasema, tupitishe katiba mpya ili tuanze kuandikia maskini katiba yao, Dhamiri inaamini, vile si busara kuweka kizuizi barabarani ndio upite, si busara kuipitisha katiba ya matajiri ili baadaye tuanze harakati za kuandikia maskini katiba yao. Linalofaa sasa ni kuua katiba ya matajiri ikiwa bado tumboni ili tutunge mimba ya katiba ya maskini. Vile wahenga walisema fahali wawili hawakai zizi moja, nayo nchi moja haiwezi kutawaliwa na katiba mbili, ya maskini na matajiri. Vile katiba ya sasa ni katiba ya matajiri, hatuwezi kuibadilisha na katiba mpya ya matajiri tena. Hekima ni kuibadilisha katiba ya matajiri na katiba ya maskini.

Kama nyenzo ya kutumalizia matatizo, katiba mpya lazima iwe ramani yakututoa kutoka lindi la umaskini wetu, itupeleke Kanaani ya maendeleo ya kila mtu. Lakini kama ramani ya kutuonyesha njia, katiba mpya lazima iwe katiba ya kanuni sio katiba ya maslahi ya makundi yenye pesa na kura. Kutupeleka Kanaani, katiba mpya lazima iangaziwe njia na kanuni za kidemokrasia na utawala bora zinazotambulika kote duniani.

Kama katiba mpya sio ya kanuni, haiwezi kuwa ramani ya kutufikisha kwenye maendeleo na demokrasia kamili.

Kwa mujibu wa falsafa hii, katiba mpya inasema Kenya haitakuwa na dini ya nchi au serikali, na dini zote zitakuwa ni sawa mbele ya katiba na sheria zake. Hata hivyo katiba mpya inazikiuka kanuni hizi kwa kuchukua Uislamu kati ya dini zote na kuihifadhi. Wakristo na wanademokrasia wakiuliza kwa nini Uislamu ukitwe katika katiba mpya, tunaambiwa kwanza tuipitishe ikiwa na mahakama ya kadhi, baadaye tuombe Mahakama Kuu yayaondoe kutoka katiba. Lakini huu ni unafiki na hila, kwani ni rahisi kutoyaweka mahakama ya kadhi katika katiba mpya sasa, kuliko kuyatoa baadaye.

Pili inasemwa, hata kama inakiuka kanuni ya usawa wa dini kuyaweka mahakama ya kadhi katika katiba, tuendelee kuyaweka katika katiba kwa sababu yamekuweko katika katiba ya sasa kwa miaka 47 tangu uhuru na hayajamdhuru yeyote. Kwa Dhamiri, ubishi huu ni sawa na kusema, kwa vile mtu ameishi na saratani au kansa ilalayo bila kuuma kwa miaka 47, hakuna haja ya kuitoa, daktari akiigundua. Mwenye kutetea saratani ya kulala iendelee kuwemo mwilini mwake, ni mtu asiyejali kufa au kupona.

Tatu inasemwa hata Wakristo wakiikataa katiba mpya hawatahepa mahakama ya kadhi kwa sababu bado yapo katika katiba ya sasa. Lakini Wakristo wakifaulu kuishinda katiba mpya kwa sababu ya mahakama ya kadhi, watatumia ushindi uo huo kuyang’oa mahakama hayo kutoka kwa katiba ya sasa.

Watu gani wataishinda katiba mpya kwa sababu ya mahakama ya kadhi na wayanyamazie katika katiba ya sasa? Isitoshe, kusema kwa sababu katiba ya sasa ina mahakama ya kadhi kwa hivyo tuyaweke katika katiba mpya ni kusema kasoro zote katika katiba ya sasa pia zihifadhiwe katika katiba mpya. Kwa nini basi tunaandika katiba mpya kama sio kumaliza kasoro zote za katiba ya sasa?

Nne, tunajua wabunge wakabila walishindwa kukita majimbo makubwa au regions katika katiba mpya. Lakini hawakushindwa kabisa. Walifaulu kupata counties ambazo ni majimbo madogo yatakayokuwa na magavana na mabunge yao madogo na bunge kubwa la seneti la kuhifadhi himaya za makabila.

Kama katika Nigeria ambako majimbo yake ya kwanza matatu yaliitwa ya kiutawala na sio ya kikabila, lakini baadaye yakazalishwa ili yapatie makabila 36 majimbo yao, hata majimbo ya katiba mpya 47, hatimaye yatazalishwa kupatia makabila ya Kuria, Teso, West Pokot na mengine majimbo yao. Jini la majimbo likitoka kwenye chupa, halitarudi ndani mpaka limeangamiza utaifa kabisa.

Tunaoishi na uhanga wa majimbo hatuwezi kuyakubali majimbo ya katiba mpya, yawe madogo namna gani au yaitwe kwa jina gani lingine.

Hapa ieleweke kwamba kupinga mahakama ya kadhi kuwekwa katika katiba mpya si kupinga yawemo nje ya katiba. Lakini yawemo chini ya sheria ya bunge kama vile dini zingine. Ivyo hivyo kupinga kuwemo kwa mahakama ya kadhi katika katiba, sio kuwa adui wa Uislamu. Lengo la kutoa mahakama ya kadhi katika katiba ni kujengea dini zote usawa dhidi ya ubaguzi na mapendeleo. Anayewapenda Waislamu ni anayezuia wasipendelewe au wabaguliwe. Ivyo hivyo anayewapenda watu wa dini zingine ni yule anayezuia wasipendelewe au wabaguliwe.

Kama mahakama ya kadhi, katika katiba mpya, swala la kuavya mimba linasukumwa na utashi wa kupata kura kutoka kwa wanawake wasomi kuliko linavyofahamishwa na kanuni muhimu ya kuhifadhi uhai wa watu wote na hasa wanyonge na watoto tumboni ambao hawana uwezo wa kujilinda na kwa hivyo sharti walindwe na katiba. Kwa mujibu huu, inashangaza kwamba katiba mpya inasema ni haramu kuavya mimba, na wakati uo huo inapatia bunge uwezo, baadaye kubatilisha kanuni ya kuhifadhia kila mtu uhai.

Dhamiri inasikitika kwamba wanasiasa wanaoomba kura za urais wanaogopa kusimamia ukweli na kanuni za uongozi bora, na badala yake kutetea maslahi ya makundi yenye kura, kama vile wanawake wasomi na Waislamu, kwa hofu ya kunyimwa kura na makundi yanayopigania maslahi yao katika katiba mpya kuliko yanavyojali ukweli na usawa.

Ajabu zaidi ni kwamba, ingawa wanaogopa kunyimwa kura na Waislamu au wanawake wasomi, wagombea urais Wakristo hawaogopi kunyimwa kura na Wakristo wenzao kwa sababu tu, Wakristo hawa wanatoka makabila yao na wamezoea kuwapa kura kiupofu.

La mwisho, Dhamiri inauliza kama kweli kuna muda wa kufanyia rasimu mabadiliko yanaodaiwa na wengi, au lazima tuipitishe na kasoro zake zote kwa kukosa muda? Hapa tunasahau, haraka haraka haina baraka na ukiona mtu anakuharakisha ufanye kitu, anatafuta kukurubuni au kukutapeli. Ukweli ni kwamba, mradi katiba mpya haijapigiwa kura ya uamuzi, kuna muda wa kuibadilisha. Katiba ya kudumu karne si kitu ambacho, watu wanaweza kulazimishiwa na watu wengine kama nchi ina uhuru na demokrasia ya kweli.

Kwa sasa bunge linalia kwamba haliwezi kuongeza muda wa masikilizano ati kwa sababu limefungwa mikono na sheria lisifungue rasimu tena mpaka ipigiwe kura na kuwa katiba mpya. Lakini sheria gani hii inayotushinikizia udikteta wakutoweza kuikarabati au kuisahihisha ramani ambayo, ikituelekeza vibaya, itatupeleka Jehanamu badala ya Kanaani?
Si Yesu alisema mtu hakuumbwa atumikie sheria, sheria ndiyo huundwa itumikie mtu? Kwa nini tusiweze kubadilisha sheria inayotukataza tuwe na katiba tunayotaka, hata kama tuna dakika moja tu ya kufanya hivyo? Hii inaonekana kama ni haraka ya wafanyabiashara laghai wanaotuharakisha tusaini katiba haramu, haraka iwezekanavyo, huku wakijua mara tu tumeipiga muhuri, tutakuwa tumejifunga na hatutaweza kurudi nyuma.

Mwisho, makanisa yanaambiwa yasipinge katiba mpya kama yalivyowasaliti Wakenya mwakani wa 2005 na 2007. Wanaopiga kelele hizi zaidi ni vyombo vya habari na hasa magazeti yale yale yaliyoungana na wanasiasa kuwasha moto wa kikabila tulio ona ukiteketeza nyoyo za Wakenya maskini. Kama katika Rwanda, kando na wanasiasa, nani mwingine alihubiri chuki za kikabila zaidi ya vyombo vya habari vinavyoyalaumu makanisa sasa? Inasikitisha kuona vyombo vya habari vikitupia makanisa mawe kama vyenyewe maasumu. Ama kweli, nyani haoni kundule.

Tamati, Dhamiri inataka kujua, tusipoweza kubadilisha katiba isiyozaliwa bado, tutawezaje kuibadilisha baada ya kuzaliwa na mifupa yake kuwa migumu? Tunapoandika katika mpya, hatuwezi kuruhusu giza liongoze mwanga.

Mara ya mwisho tulipigia katiba mpya kura, Wakenya walisema, bendera ifuate upepo. Sasa, watahadhari kabla ya hatari. Heri nusu ya shari kuliko shari kamili.

4th April, 2010.

About SG

Secretary general of Chama Cha Mwananchi. This blog www.chamachamwananchi.wordpress.com, is based in Sweden.

Discussion

No comments yet.

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Advertisements
%d bloggers like this: