//
you're reading...
Uncategorized

KENYA LEADERS PROPAGANDA

Propaganda Na Vita Vya Katiba Mpya

Vile tunavyokaribia kupigia katiba mpya kura ya uamuzi, Dhamiri ya Sauti ingetaka kuwatahadharisha Wakenya kwamba vita vya ndio na la kwa katiba mpya havitapiganwa kwa ukweli, vitapiganwa kwa propaganda.
Lakini propaganda ni kitu gani?
Kwa kifupi, propaganda ni habari za uongo au nusu ukweli zinazofanywa zionekane kama ukweli na kutumiwa kuwashawishi watu wabadilishe mawazo au wachukue msimamo fulani kuhusu jambo fulani.
Iwe hivyo kama ilivyo, Dhamiri ingetaka wananchi wajue kuwa vita vya propaganda ni vita vya “asiye na mwana na aeleke jiwe” na “mwenye nguvu mpishe.”
Propaganda hutumiwa katika vita moto, vita baridi, vita vya kisiasa na vita baina ya dini wakati watu wanahisi lazima wapate ushindi kwa vyovyote vile.
Katika nchi yetu vita vya propaganda vilitumiwa sana na Wazungu dhidi ya wapiganiaji uhuru wa Mau Mau. Kwa mfano propaganda za wakoloni zilidai Mau Mau walikuwa wala watu.
Vita vingine vilivyopiganwa sana kwa propaganda vilikuwa ni vita baridi kati ya mataifa ya kibepari na mataifa ya kijamaa. Katika vita hivyo wajamaa walichorwa kama maadui wa uhuru, na mabepari kama wala watu.
Wakati wa kutafuta uhuru wa pili, wale wote walipigania uhuru na haki walichorwa kama waasi na makomunisti waliostahili kuteswa na kuuawa ili nchi ipate utulivu, amani na maendeleo.
Kando na propaganda za serikali, propaganda za ukabila hudai Wakikuyu wote ni wezi, Wajaluo hawatoshi kutawala nchi, Wakamba wamelewa mapenzi, Waluhya hawaaminiki, Wakalenjin hawaachi kuomba na kadhalika.
Majuzi propaganda zilitumika sana wakati wa kura ya uamuzi ya 2005 na tena katika uchaguzi mkuu wa 2007.
Vyombo vinavyotumiwa kupigia propaganda vinakuwa ni pamoja na magazeti, radio, runinga, makampuni yanayotafiti maoni kama Synovate, mahubiri na mikutano ya wanasiasa. Lakini vyombo vya habari vikishirikiana na makampuni ya maoni ndiyo hueneza propaganda kuliko wengine wote.
Kwa mfano, wakati kampuni ya Synovate inahoji watu 2000 tu kuhusu katiba mpya na kutoa maoni yao kama ya watu wote wa nchi milioni 40, ripoti yao ni propaganda inayotolewa kama ukweli.
Katika uchaguzi wa 2007, sababu moja ya vita kuzuka ilikuwa kwamba kura nyingi za maoni zilikuwa zimetangaza Raila na ODM kama washindi wa uchaguzi ambao ulikuwa haujafanyika bado.
Wakati ushindi huu ulikosekana katika matokeo ya uchaguzi, watu waliamua kura zimeibiwa na serikali na kuanzisha vita.
Majuzi tumeona kampuni ya Synovate ikitangaza maoni ya asilimia 64 ya watu 2003 iliowahoji kama maoni ya watu milioni arobaine wa Kenya wakisema ndio kwa katiba mpya. Wakati uo huo kampuni hio ilidai asilimia 17 ya 2003 waliosema la pia ilikuwa asilimia 17 ya wakenya wote walioshindwa kwa kusema la. Ijapokuwa lengo la kura hii ya maoni ilikuwa ni kushawishi watu wa la wakubali kushindwa na waiunge mkono katiba mpya, ushindi bandia huu wa ndio ukiendelea kutangazwa kama ushindi kamili, halafu usipatikane katika matokeo halisi ya kura ya uamuzi, watu wa ndio watasema kura zao zimeibiwa na wazushe fujo.
Ingawa watu wa ndio watasema maoni ya Synovate ndio ukweli wa mambo nchini, ukweli ni kwamba maoni ya watu 2003 hayawezi kuwa ndio maoni ya watu milioni arobaine wa Kenya. Hata kama haina uwezo wa kupigisha kura za maoni za aina hii marufuku, Dhamiri itasema ni jinai kupotosha ukweli namna kura hizi za maoni zinavyofanya.
Propaganda zingine zinazosambazwa na magazeti pamoja na runinga nyingi ni zifuatazo:
Propaganda ya kwanza ni, kama katiba mpya ni chongo, kwa vile katiba ya sasa ni kipofu, nchi haihitaji katiba ya macho mawili. Kwa hivyo, badala ya kupatia katiba mpya macho mawili ili ione vizuri kule itupelekako, tuipigie kura kwa sababu chongo ni bora kuliko kipofu.
Propaganda ya pili ni,. kwa sababu tumekuwa na mahakama ya kadhi na hayajatatiza Wakristo, kanuni ya kutenganisha dini na serikali na kuhakikishia dini zote usawa si muhimu tena na kwa hivyo ni sawa kuyakita mahakama ya kadhi katika katiba mpya hata kama kufanya hivyo kutaukweza uislamu juu ya dini zingine.
Propaganda ya tatu ni, ingawa katiba ni mkataba wa kulinda maslahi ya watawaliwa wasinyanyaswe na watawala, ni sawa kabisa kuipigia kura hata kama ina kasoro zitakazowasaidia watawala kuwakandamiza wananchi. Na ijapokuwa watawaliwa watapoteza haki zao kwa kuidhinisha mkataba wenye kasoro, watawala wanahimiza wananchi wapigie kura mkataba huu na kasoro zake, halafu baadaye waombe watawala wawaondolee kasoro hizo. Ni kama kondoo asihiwe na simba kuingia katika nyumba yake halafu aulize simba amfungulie mlango atoke.
Propaganda ya nne ni, kukitwa kwa mahakama ya kadhi katika katiba mpya hakuwahusu Wakristo ndewe wala sikio. Ukweli ni kwamba, tofauti na wachungaji, makasisi au mahakama ya wazee vijijini wanapofunganisha ndoa au kufanya kesi za mipaka au urithi, makadhi wa mahakama ya kiislamu watalipwa mishahara yao na kodi yangu na yako hata kama sisi si Waslamu. Kutumia kodi ya wananchi kugharamia shughuli za dini moja tu nchini si haki hata kidogo.
Ukweli ni kwamba kwa kugharamia mahakama ya Kadhi, Wakristo wanakula pilipili yake na ndio sababu inawaasha.
Propaganda ya tano ni,. kwa sababu tumengojea katiba mpya kwa muda mrefu, lazima tuwe na katiba mpya sasa hata kama ina kasoro au upungufu gani. Hii ni sawa na kutwambia tule chakula chenye sumu kwa sababu tu tumekuwa na njaa kwa muda mrefu.

Propaganda ya sita ni, katiba mpya ni nzuri kwa mwewe kama ilivyo nzuri kwa mwanakuku. Ukweli ni kwamba kama kuku anauziwa katiba na mwewe, hiyo katiba haiwezi kuwa nzuri kwake.
Propaganda ya saba ni,. ijapokuwa haigawii maskuota shamba wala haiotoi mwelekeo wa kumaliza umaskini na ubepari nchini, bado katiba mpya ni katiba ya maskini.
Propaganda ya nane ni, kwa sababu katiba mpya ina kansa ya mahakama ya kadhi, na katiba ya sasa bado ina kansa hiyo, hakuna haja ya kutoa kansa hiyo mwilini mwa katiba mpya.
Propaganda ya tisa ni, mahakama ya kadhi hayatekelezi sharia au sheria za kiislamu. Ukweli ni kwamba sheria za kiislamu zinazoshughulikia ndoa, urithi na talaka ni sehemu ya sharia.
Propaganda ya kumi ni, kwa sababu wanawake wanaavya mimba sasa kinyume cha sheria, heri katiba mpya iwaruhusu kuavya mimba kisheria.
Propaganda ya kumi na moja ni, kwa sababu ni Raila anaongoza kampeni ya kusema ndio kwa katiba mpya, itakuwa ni haki yake kuongoza nchi katiba mpya ikipita.
Propaganda ya kumi na mbili ni, watu wote wanaopinga katiba mpya wanafanya hivyo kwa sababu sawa na zile za Moi na Ruto. Si hoja watu ambao wamekuwa wakipigania uhuru wanapinga katiba kwa sababu haina sura za kupigana na umaskini, ufisadi na zaidi ya yote ukabila ilhali katiba mpya imeandikwa kwa damu ya wahanga wa ukabila na siasa za majimbo.
Propaganda ya kumi na tatu ni, wasemao la na wale wasemao ndio wakiandikiana mkataba au MOU, serikali itauheshimu na kushughulikia mabadiliko ya katiba mpya baada ya kupita.
Ukweli ni kwamba vile Kibaki hakuheshimu MOU yake na Raila, hata sasa, hataiheshimu MOU ya serikali na upande wa la.

Propaganda ya kumi na nne ni, mradi walio wengi wanasema ndio kwa katiba mpya, katiba hiyo ni sawa tuipitishe kwani walio wengi na wanaoshinda hawakosei. Lakini hata kama methali husema wengi wape, hiyo haimaanishi wengi hawakosei. Mara nyingi wanaoshindwa ndio wenye haki. Haki wakati wote haishindi au Yesu hangesulubiwa.
Wachache hupigania na kusimamia ukweli sio ili washinde lakini kwa sababu penye ukweli ndipo penye Mungu.
Propaganda ya kumi na tano ni, wanaosema la kwa katiba mpya si wazalendo. Lakini katika nchi hii na nchi zingine, mara nyingi wasemao la ndio wazalendo kuliko wasemao ndio.
Siku za mwongo ni arobaine na ukweli ukidhihiri uongo hujitenga.

Koigi wa Wamwere.
26/4/2010.

About SG

Secretary general of Chama Cha Mwananchi. This blog www.chamachamwananchi.wordpress.com, is based in Sweden.

Discussion

No comments yet.

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Advertisements
%d bloggers like this: