//
Ndoto ya CCM

Ndoto Ya CCM Ni Ndoto Ya Mwananchi.

Mheshimiwa Koigi wa Wamwere kupitia Makao Makuu ya CCM, 17/1/07

Kila chama huwa na sababu yake ya kuanzishwa. Kuna vyama huanzishwa kuwamilikisha matajiri, wakubwa na viongozi serikali na hatimaye mali ya nchi. Vyama vingine huasisiwa kama jukwaa la wenye kuvianzisha na bado vyama vingine huundwa ili vipiganie maslahi ya makabila fulani.

Chama cha Mwananchi au CCM kimeanzishwa kwa sababu tatu muhimu.

Kwanza, kama jukwaa la maskini kupigania maslahi yao. Pili kiwe tumbo la kufugia ndoto ya mwananchi mpaka itakapozaliwa. Tatu, CCM imeanzishwa kwa lengo la kupigania serikali ya wananchi walio wengi ambao ni maskini, wasio nacho.

Wakati mwafrika alitegemea uwindaji kwa chakula, kila mwindaji alikwenda mawindoni na mbwa wake na mbwa aliyempata mnyama ndiye aliyegawiwa sehemu kubwa ya windo lililopatikana. Zama zile hakuna aliyekwenda mawindoni bila mbwa wake.

Siku hizi vyama vya siasa pia ni mbwa wa kuwindia mamlaka na rasilimali na hakuna watu au wanasiasa wanaoingia uwanjani wa siasa bila chama au mbwa wao wa kuwindia. Wanaoingia siasani bila mbwa wao, windo likipatikana, wao ndio hupata mikia, makanyagio au hurudi nyumbani bila kitu.

Katika zama zetu, maskini na matajiri hung?eng?ania mawindo ya nchi siasani. Mpaka wa sasa tajiri amekuwa akifanikiwa katika kinyang?anyiro hiki kuliko maskini kwa sababu hwenda mawindoni na mbwa wake wakati maskini hwenda mawindoni bila mbwa wake au kama mbwa wa tajiri. Kama mbwa wa tajiri, kile anachogawiwa mawindoni mara moja huchukuliwa na tajiri wake.

Waasisi wa CCM wanataka maskini wa Kenya awe na mbwa wao wenyewe waendapo mawindoni na mbwa huyo atakuwa ni Chama cha Mwananchi. Kama mbwa wa maskini, CCM atamwindia, apiganie maslahi yake na wakati huo huo amhami maskini asidhuriwe na maadui.

Sababu ya kuundwa CCM ni kuzalisha ndoto ya maskini.

Tangu nchi yetu itekwe nyara na sisi tutawaliwe na kufukarishwa na mkoloni, ndoto yetu imekuwa ni kuupata tena utu wetu, uhuru wetu na nchi yetu. Hii ndio ndoto waliopigania, waliofungiwa, waliotesewa na kuuliwa Mau Mau pamoja na mashujaa wengine wa uhuru. Wakati tulipata uhuru, ndoto hii ilistahili itimike kwa watu wote lakini ilisalitiwa na kuzaliwa kwa watu wachache ? wasomi, viongozi na waliokuwa manyapara wa mzungu. Alipokuja Moi, usalati wa ndoto ya uhuru uliendelea kama katika wakati wa Kenyatta na unavyoendelea hadi sasa. Utawala wa kiimla wa mtu mmoja na chama kimoja ndio uliokuwa kilele cha usaliti wa ndoto ya uhuru na maskini walio wengi. Wengine walipoona usaliti huu waliamua kupigana nao na kwa miaka mingi wakastahimili, kizuizi, vifungo, kunyimwa kazi, mateso, uhamisho na vifo.

Baada ya miaka mingi ya taabu, udikteta wa Kanu ulianguka lakini ndoto ya maskini haikutimia. Ndoto ya maskini ingali bado kwa sababu, wakati wa vita vya Mau Mau, maskini alitazama waafrika wasomi,wafanyabiashara, viongozi na walioinuka kidogo wamwokoe. Hivyo hivyo wakati wa kupigana na udikteta wa Kanu, mwananchi alimtazama kiongozi na tajiri amuokoe. Maskini alipopigana katika vita vya Mau Mau na vya ukombozi wa pili, alipigana kama mbwa wa tajiri. Windo lilipopatikana
hakugawiwa kitu. Hata sasa, maskini anaposhirikishwa siasa, hasa za uchaguzi, anashirikishwa kama mbwa wa tajiri. Hana matamanio ya kupata kitu mpaka apigane akijipigania mwenyewe, aende mawindoni akiwa na mbwa wake.

CCM imeanzishwa kuendeleza vita vya ndoto ya mwananchi kuanzia pale walipoachia mashujaa wa vita vya ukombozi wa pili. Leo ni wazi kwamba kama mwananchi atapata ukombozi wake wa kiuchumi, sharti awe na chama chake mwenyewe! Chama cha Mwananchi. Vingine, mwanachi atakufa maskini kama mtegemea cha nduguye.

Itakaposhika hatamu za serikali, kazi kubwa ya CCM itakuwa ni kuvikamilisha vita walivyopigana Mau Mau na vita walivyopigana mashujaa kama J.M. Kariuki, Pio Gama Pinto, Jaramogi Oginga Odinga, Bildad Kaggia, Elija Masinde, Masinde Muliro, Bishop Muge, Ntai wa Nkurai, Karimi Ndutho na wenngine wengi.

CCM ikiunda serikali, itaumwinua na kumrudishia mwananchi utu na heshima yake. Itaunda undugu wa Wakenya wote kwa kuiua saratani ya ukabila. Itamtimizia mwananchi mahitaji yake ya kupata kazi, shamba, chakula, maji, matibabu, nguo, elimu, usalama na usafiri nafuu. Itamalizia nchi ufisadi na wizi wa mali ya umma. Itashughulikia maridhiano ya kitaifa kupitia Tume ya Haki, Ukweli na Maridhiano. Itamshirikisha mwananchi kikamilifu katika uongozi wa serikali ya nchi. itamrudishia mwafrika utamaduni na lugha zake ili asiendelee kuwa mtumwa wa mataifa ya nje. Itapigania ndoto ya kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki na hatimaye muungano wa Afrika nzima.

Kimtazamo, ndoto ya CCM ndio ndoto ya nchi, ndoto ya walio wengi, ndoto ya uhuru na ndoto ya Mungu alipomuumba mtu na kumueka duniani afurahie matunda yake.

Tusipoipigania ndoto hii ya CCM, sisi tuliopigania uhuru wa pili na babo tuna nguvu, tutakuwa tumejisaliti wenyewe, tumemsaliti Mungu, nchi, Mau Mau, mashujaa wote wa uhuru wa pili, wananchi na watoto wetu na hakuna atakayetusamehe.

Bila shaka, ndoto hii itapingwa na wengi wasiomtakia mwananchi wa kawaida mema. Tunajua wataibatiza maneno mengi maovu ya kuikashifu. Lakini kama Martin Luther King Jr. alivyosema: lazima tutashinda! We shall overcome.

Mheshimiwa Koigi wa Wamwere kupitia Makao Makuu ya CCM, 17/1/07

Discussion

No comments yet.

Leave a comment